“Kifo Cha Mende Cha Isubiri Jubilee” – Moha Jicho Pevu

January 18, 2016

mohaWalisema kifo cha mende ni kulala chali. Hakika aliyesema haya hakukosea. Serikali ya Uhuru Kenyatta kwa mtazamo wa wengi ni kama mende anayesubiri kifo chake mwaka wa 2017 kutokana na ahadi zake tasa.
Wiki iliyopita katika ziara yake mjini Mombasa, Uhuru Kenyatta aliwadhihirishia wakenya kwamba yeye hana doa la uongozi pale alipoingia kaunti ya Gavana wa Mombasa Hassan Ali Joho na kufanya mambo kinyume na mgeni aliyepewa chumba cha kulala na kukigeuza kuwa duka la vikaragosi.
Kwa zaidi ya wiki mbili rais aliendeleza shughuli zake bila ya kumhusisha Gavana Joho — labda kutokana na kile kinachotajwa na wadadisi wa masuala ya kisiasa kama chuki dhidi ya Gavana na Pwani kwa kumnyima kura mwaka wa 2013.
Ni dharau kwa mtu kuingia kwa jirani na kuanza kujipakulia chakula bila idhini ya mwenye nyumba. Katika uwanja wa Shika Adabu huko Likoni, Uhuru Kenyatta alidhihirishia wakenya hofu waliokuwa nayo tangu na mwanzo pale aliponyamaza kimya seneta wa Nairobi Gideon Mbuvi, almaaruf Mike Sonko alipoanza kumfokea Joho.
Zamu ya Uhuru Kenyatta ilipofika yeye pia alianza kwa kuwataka wapwani wafahamu kuwa hawakumpigia kura. Na kwamba ni sharti maskwota wasio na mbele wala nyuma walipe laki moja na elfu themanini na mbili licha ya vilio vya viongozi wa pwani.
Iwapo wapwani watalipa, japo najua hawataweza, basi ina maana kuwa kuna mtu atatia shilingi milioni mia saba mfukoni kama faida ya Ardhi ya Waitiki. Majibu ya Gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho yalikuwa ya hekima na busara.
Kwanza alimkosoa Uhuru Kenyatta kwa kile alichokiona kama dharau ya kutomjulia hali licha ya kuingia ndani ya boma yake na pili hila za jubilee dhidi ya maskwota. Joho aliwataka wana-jubilee wafahamu kuwa wapwani hawawezi nunuliwa, wala tishio za baadhi yao mbele ya rais ni sawia na kumpigia mbuzi gitaa.
Majuzi Mgombea kiti cha ugavana kwa tiketi ya Jubilee Suleiman Shahbal alifoka na kutamka kuwa Jubilee itaiba kura kuhakikisha imo kileleni. Hii ndio demokrasia ya kijambazi ya Jubilee. Kuiba kwao ni kama ibada. Ibada ya kuiba hadi kiama.
Je, ni njama gani zinazopangwa na wabakaji wa demokrasia dhidi ya maamuzi ya wakenya mwaka wa 2017 hususan pwani ambayo imedinda kucheka na jubilee Ni vitu vitatu tu vilivyosalia katika meza ya jubilee!
Kikundi cha MRC
Kwa kipindi cha miaka mitatu, Uhuru Kenyatta ametawala bila ya madai ya Mombasa Republican Council (MRC) kuchipuka tena. Huu mwaka, kwa sababu Uchaguzi mkuu unanukia, utaskia maswala ya MRC ikichipuka tena huku watu wasio na hatia wakizidi kudhulumiwa kwa kutuhumiwa kuwa washirika la kundi haramu.
SGR na tarakilishi
Huu utakuwa mwaka wa vihoja. Mwaka huu, jubilee imeshindwa kujenga viwanja vitano vya mpira kama ilivyoahidi na hata kushindwa kuwapa watoto tarakilishi.
Huu utakuwa mwaka wa Jubilee kufufua maswala haya ilikujifanya mkombozi. Serikali pia itaharakisha ujenzi wa reli ya SGR ilikumaliza kabla ya mwaka wa 2018.
Vitambulisho
Ni wazi kwamba ngome za upinzani zinazidi kunyanyashwa na wasajili wa vitambulisho kwa lengo la kuwazuia kupiga kura mwaka ujao na kufanya maamuzi ya busara.
Sheria hii ya kijambazi inazidi kutekelezwa na baadhi ya watu Fulani walio na hila ya kutwaa ushindi kimabavu. Mwaka uliopita nilitoa lalama zangu binafsi na kuelezea masaibu ya dadangu ambaye mwaka mmoja sasa bado hana kitambulisho licha ya kufuata sheria zote.
Baadhi ya majumba ya Huduma Center bado yanazidi kukashifiwa kwa uozo wa kutoa vitambulisho kwa wale wanaoonekana kama wenye nchi na bora zaidi ya wakenya wengine sawia na tamthilia ya shamba la wanyama na kuwanyima wengine kwa misingi ya kikabila, dini na chuki za kibinafsi.
Wiki ijayo, Inshaallah, nitazidi kuelezea hila zinazotumiwa na wanafiki ndani ya serikali kuwanyima wakenya haki zao za kimsingi. Nitamalizia na kibwagizo cha gavana wangu Ali Hassan Joho- “MWENYE NGUVU AKIJA STEDI NAYE”
sde

Leave a Reply

Your email address will not be published.Don't Miss