Jicho Pevu’s Moha: Kama Unampenda Uhuru Kenyatta…

February 20, 2017

By Mohammed Ali

Kauli mbiu ya William Samoei Arap Ruto ya kuwarai jamii ya wakikuyu kumpigia kura Uhuru Kenyatta ni: “Kama mnampenda Uhuru Kenyatta basi mpigieni kura Agosti 8”.

Kuiomba jamii moja kuonyesha mapenzi yao kwa mtoto wao – kwa sababu anatoka kwenye kabila lao- kamwe sio siasa komavu. Hii ni siasa ya kukuza mbegu za chuki na uhasama kati ya jamii zingine – na kushurutisha jamii mbili kuona jamii hizo zingine kama hayawani.

Tangu nizaliwe sijawaona Daniel Arap Moi na ndugu Mwai Kibaki wakipiga siasa kwa lugha yao kama njia ya kuwarai wapiga kura.

Hii yenu ya kuzungumza lugha ya nyumbani kati kati mwa jiji la Nairobi na viunga vyake ni hatari kwa usalama. Kwa Rais kutumia lugha yake ya nyumbani ni sawia na kuwalisha kiapo ki-siri kuwa wakishindwa wataumia sana.

Naye naibu wa rais, ndugu William Ruto anadhani waKenya wamesahau mbegu ya chuki iliyokuzwa mwaka wa 2007 baina ya jamii ya wakikuyu na wakalenjin. Amesahau kuwa bado tunawakumbuka kina mama waliochomwa katika kanisa la Kiambaa. Kwamba tunakumbuka zaidi ya watu elfu moja waliouawa wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi.

Leo hii wawili hao hawana cha kujivunia ila kupiga kampeni za mapenzi ya Uhuru Kenyatta. Ukweli wa mambo ni kwamba mie binafsi sipendi uongozi wenu wa fitna, ufisadi, wizi wa ardhi, dhulma, ukabila, chuki na ukiritimba.

Mnajifanya kupenda taifa hili zaidi yetu ila mwatuangamiza pamoja na vizazi vijavyo kwa ajili ya ubinafsi wenu. Ndugu yangu Ruto, najua moyo wako vizuru. Najua mapenzi yako kwa marafiki zako — lakini kumbuka nilikuandikia barua miaka ya nyuma na kukuonya.

Waswahili wanasema tembea na muuza marashi unukie marashi. Hao unaotembea nao hawanuki marashi ila chuki na uhasama dhidi yako. Hao unaotembea nao wanakutumia kama daraja ya uchaguzi. Utatemwa kama Big G mwezi wa Septemba iwapo mtashinda — japo ushindi wenu ni kama kutia gunia upepo.

Kila ninapo zungumza na viongozi wakuu kutoka kitengo hicho kinachojiita ‘UTHAMAKI’ wao hucheka na kusema kuwa hawatakubali uwe Rais mwaka wa 2022 kwa maana umekuwa makamu wa Rais kwa vipindi viwili. Kila ninapopiga gumzo mtaani wanakulaumu wewe kwa kuharibu serikali ya Uhuru Kenyatta. Leo hii unaowapigania wamenoa kisu dhidi yako, watakukimbiza kila kona, kesi zako zote zitafufuliwa, utatemwa, utajihisi mgonjwa, utasalia yatima na kufa kifo cha pole pole.

Uliowapigania watakuruka futi mia moja, utachekwa na kuachwa ukilia wewe na familia yako. Tayari unawindwa mitandaoni na hao ‘36 Beggars’ ambao wanapatiana siri zako nje ili uanze kutafunwa pole pole.

Ya Abby si haba japo aliyefichua sakata hiyo alikosea maana hakuna aliye mkamilifu mbele ya Mungu. Japo sikufurahishwa na jambo hilo bado nakuombea rabana ufungue macho. Mimi nakukumbusha tu kwa sababu urafiki ni kitu cha maana, japo kila mmoja ameshika njia zake, marafiki wazuri hukumbushana na kupeana ushauri.

Langu ni hilo Ndugu yangu William Ruto. Kama kweli uko radhi utapewa kiti cha UTHAMAKI 2022 basi anza kampeni zako kwa kusema kama unampenda William Ruto kata kura. Ulikuwa kipenzi cha watu mwaka ya 2007, ulipendwa sana kwa kuwa na msimamo na kusimama na wakenya, leo hii nashangaa hawa watu wamekulisha nini?

Uhuru Kenyatta hana muda na wewe anajua akifaulu raundi ya pili basi wewe chako ki motoni maana hana hasara kwani ni kipindi chake cha lala salama.

Kumbka kuwa mwaka wa 2013 karata ya kumwondoa Raila Odinga uongozini ulianza kupangwa na Mwai Kibaki akisaidiana na wafuasi wake kama kina Julius Karangi. Ilisemekana kuwa Raila alikuwa waziri mkuu na alikuwa na nguvu si haba.

Kumwondoa uongozini, mtu kama wewe ulihitajika. Waliamua kukutumia kupasua ODM ili nguvu zako zisaidie Uhuru Kenyatta kushinda uchaguzi. Leo waliompangia Raila ndio unayopangiwa wewe. Julius Karangi amerudi kuendeleza kampeni za Uhuru Kenyatta. Zamu ni yako sasa. Kwa ufupi ni “MTUMIENE RUTO KULINDA UTHAMAKI”.

Utatumiwa kisha mahakamani baadaye kujibu mashtaka dhidi ya shule ya Langata, wizi wa ardhi, mtoto Abby, ardhi ya Karen, Hoteli ya kifahari unayojenga huko Mombasa mkabala na Hoteli ya Flamingo, mauaji ya Yebei, vitisho dhidi ya Boniface Mwangi, ardhi unaodaiwa kunyakua Eldoret na kufunga barabara ya Ikuli karibu na Golf Club… Yaani kwa ufupi jinsi wanavyofufua wafu kupiga kura ndivyo utakavyo fufuliwa kila aina ya kesi.

Ndugu William, Koma hizo siasa za kama unampenda Uhuru Kenyatta chukua kura. Wewe binafsi humpendi mbona washurutisha wakenya wampende? La mwisho, ningependa kukujulisha kuwa hata jamii ya wakalenjin imechoka.

Wanajua wazi kuwa mtoto wao Samoei atasulubiwa na watu anaowapigania. Wana machungu na hata kuniambia nikuelezee. Jibu langu kwao nikuwa William – ambaye ni rafiki yangu — pia mimi humwona tu magazetini na kwenye Runinga. Mwisho kabisa kumbuka Moi kwa kipindi cha miaka 24 uongozini hakupigiwa kura.

Je, wewe ni nani upigiwe? Akili kichwani!

Leave a Reply

Your email address will not be published.Don't Miss