Jicho Pevu’s Mohammed Ali: ‘Rais Uhuru, Kipindi Cha Lala Salama Kimewadia’

January 16, 2017

By Mohammed Ali

Zimesalia takriban miezi saba wakenya wafanye maamuzi yao.

Shida ni kuwa maamuzi haya yatatatuliwa na watu wachache ndani ya serikali. Watu walio na nyoyo za kutu na wenye chuki dhidi ya utawala wa kabila zingine.

Watu hawa watasubiri wakenya wapige kura kisha wao wajifanye kuhesabu kura hizo kwa niaba ya wakenya. Tayari serikali ya Uhuru Kenyatta imeonyesha dalili ya kutokubali maamuzi na matokeo ya Agosti mwaka huu kwa kuanza kujiandaa vilivyo. Je, wanajiandaa vipi?

Mutahi Ngunyi

Yeye ndiye aliyezalisha jina la Tyranny of Numbers. Sasa amekuja na jingine jipya la kusema kuwa nafasi ya waziri mkuu itaundwa tena baada ya uchaguzi. Hapa ule msemo wa umbwa akibweka mtafute mwenye mbwa unajiri.

Mutahi na elimu yake ya kikabila anazungumza kwa niaba ya serikali iliyomwajiri. Serikali iliyomwonjesha pesa za ufisadi za NYS kabla ya kujitakasa na kujifanya kuregesha. Duru zinatuarifu kuwa Mutahi anashirikiana na jamaa mmoja kwa jina la Michuki ndani ya makao makuu ya NYS Nairobi kuandaa mbinu ya kuibia miungu zao kura.

Mutahi ni miongoni mwa wale waliotajwa kwa tuhuma za ufisadi. Kenya hii ni nchi ya ajabu. Wafisadi, watapeli, wahuni na wauaji ndio wanaowapa chakula ya kiroho na mawaidha wakenya. Mutahi Ngunyi msemaji wa msimu, msemaji wa chochoro nitarejea hivi karibuni. NYS ni jumba lililojaa uozo.

Silaha

Je wakenya mna habari serikali yenu badala ya kuwapunguzia bei ya vyakula inanunua magari ya usalama? Badala ya kuwalipa madaktari inafanya mahaba na pesa zetu? Kuwa badala ya kujenga nchi inabomoa nchi? Magari haya si ya kuwabeba nyinyi na kuwapeleka maharusini.

Magari haya ni ya kuwakimbiza kama sungura, kuwawinda na kuwaangamiza mtakapojitokeza kupinga matokeo ya uchaguzi. Sijaona serikali inayowafanya watu wake maskini, na badala ya kuwasaidia inanunua vifaa vya vita utadhania tuko Syria.

Ujumbe wa amani

Amani ni umbea ya walio mamlakani, hatumo kwenye vita. Tangu Kenya kupata uhuru imekuwa ni taifa la amani — na itazidi kuwa na amani kwa nguvu zake Maulana. Wezi wote Kenya sasa wanahubiri amani maana wanajua siku za wezi wote Kenya ni Agosti mwaka huu.

Baada ya kubaka taifa sasa kizazi cha ufisadi kinataka kuwaambia wakenya wapige kura kwa amani ilhali wana nia na njama chafu dhidi ya Kenya na wakenya. Mtahubiri vipi amani wakati katika utawala wenu wakenya wengi wameuawa?

Mmesahau mauaji ya Muchai, Jacob Juma, Sheikh Aboud Rogo, Makaburi, Wakili Willy Kimani na wenzake miongoni mwa watu wengine wengi waliouawa na serikali hii ya mtu mle mtu? Kenya imejaa amani tele.

Joho/Kingi

Serikali ya kitoto huwa na matendo ya kitoto. Eti kwa sababu Gavana wa Mombasa amemkosoa Uhuru Kenyatta kuhusiana na miradi yake tasa, sasa wanaodhani wanamiliki Kenya wameanza kasumba zao za kitoto kwa kuwaondoa walinzi wa Joho na Kingi.

Je, kuna nia ya kuwaangamiza wawili hawa? Natumai hamtawaondoa maafisa wa polisi wanaoshika doria katika ngome za upinzani eti kwa sababu watu wa huko hawacheki na mbuzi. Serikali inafaa ikumbuke kuwa chochote kitakachotokea dhidi ya magavana hao wawili basi damu hiyo itakuwa mikononi mwake.

Chaguzi Dijitali

Jitayarisheni maana wafu watapiga kura. Ndio! marehemu babako, mamako, dadako, ndugu yako na wajomba zetu watapiga kura kwa niaba ya wanafiki wachache wanaotaka kunyonya damu ya kila mkenya. Jamani wapigisheni kura maiti lakini mkumbuke wote watafufuka wakati wa kupinga dhulma hizo agosti.

Asasi za Usalama

NIS, Polisi, Jeshi, NYS na vyombo vyote vya usalama kwa mapenzi ya taifa hili kaeni mbali na maamuzi ya wakenya mwaka huu. Miaka ya nyuma NIS ilitajwa pakubwa kuhusika na udanganyifu wa uchaguzi wa mwaka wa 2007, wao ndio chanzo kikuu cha ghasia za baada ya uchaguzi kwa maana waliamua kuhesabu kura za wakenya badala ya tume ya uchaguzi ya marehemu Kivuitu.

Katika uchaguzi wa mwaka huu tayari dalili za asasi hizi kuhusika zinaanza kuonekana. Kwa mara ya kwanza nawasihi maana najua hamtashinda nguvu za wakenya dhidi ya maamuzi yao. Kaeni mbali na maamuzi ya wakenya.

Amina Mohamed

Dadangu najua unatafuta kiti cha mwenyekiti wa jumuiya ya Afrika. Wanaokupigia debe ni wahuni wachache wanaotaka upate kiti hicho ili wakiiba kura wewe utumiwe kupinga vilio vya wakenya.

Nakukumbusha kuna jamaa alikuwa akijiita Jean Ping alidhulumu Raila Odinga mwaka wa 2007 na kusema jumuiya ya Afrika iko nyuma ya ushindi wa Kibaki. Jamaa huyo sasa yuanyolewa bila maji huko kwao baada ya kupigania kiti cha urais na kufanyiwa alivyomfanyia Raila Odinga. Malipo ni papa hapa duniani.

Dadangu usikubali kutumiwa, hawa watu hawana utu, hawaogopi Mungu. Hawa watu wanataka kukutumia kama daraja ya wizi wa kura. Hamna jumuiya ya afrika, kama ni jumuiya ni jumuiya ya wahalifu sugu na wabakaji wa demokrasia.

Joseph Nkaissery

Wewe umejifanya Mike Tyson wataka kupiga kila kuta ngumi. Leo sina la kukuambia ila kukukumbusha tu hamna nguvu kama nguvu ya wakenya. Zaidi ya hayo nakuombea Mungu mwaka huu akupe hekima ya kufanya kazi kiheshima. Kumbuka kulikuwa na Biwot kabla yako, utachemsha ukijifanya kujua zaidi ya Kenya.

Leave a Reply

Your email address will not be published.



Don't Miss