‘Buriani Ndugu Jacob Juma’- Moha Jicho Pevu

May 25, 2016

mohaBy Mohammed Ali
Buriani ndugu Jacob Juma Lukhoba. Wakenya wana machungu kutokana na kifo chako.
Juma, visa vya hapa na pale vilijitokeza maishani mwako — sawia na binadamu yeyote dunia kwani hakuna aliyekamilka.
Ingawa ulikuwa na changamoto zako, wakenya wameishia kukuvulia kofia — baada ya kifo chako tatanishi.
Wengi wanaulizia maswali huku wakitaka kuwajua makatili waliokufanyia unyama huu.
Maswali bado yanaulizwa hata baada ya wewe kuzikwa, lakini serikali imekuwa kama bata. Tayari idara ya usalama nchini imeanza kujiharia huku ikitoa taarifa za kutatanisha. Baada ya sisi kuuliza maswali, siku sita baada ya kuuawa kwako, sasa makao makuu ya CID inasema imefaulu kupata maganda mawili ya risasi
Uliowataja hadharani mitandaoni kwa kile ulichokitaja kama njama ya kutaka kukuua, bado wapo — polisi hawajabisha hodi kwao angalau kuulizia tu!
Ingawa baadhi ya jumbe zako zimeanza kutoweka mitandaoni, bado twazisoma jumbe zako tukisubiri haki kutendeka.
Majangili hawa wafisadi wamefaulu kukuua kinyama kwa sababu ya ushahidi uliodai kuwa nayo dhidi yao.
Nimesikia mengi tu tangu kufa kwako. Nimesikia kuhusu kikosi fulani cha watu nane, na kisicho na jina. Nimesikia pia kuhusu kemikali fulani inayotiwa kwenye maziwa pamoja na uamuzi wako kulingana na swala hilo.
Nimesikia mengi kuhusu mauaji yako, lakini kwa sasa langu ni kutega sikio tu hadi pale wakenya watakapojua ukweli.
Mjuzi wa ushahidi huu wote ni Mwenyezi Mungu kwani kutegemea polisi wetu kufanya uchunguzi ni kama kutia gunia upepo.
Sina imani na afisi ya Ndegwa Muhoro kwani imehusishwa na sakata nyingi tu.
Afisi ya Inspekta Jenerali wa polisi ni nyengine iliyojaa vihoja na viroja. Ni afisi ya kutisha wakenya hata wanapochafua hewa kutokana na mlo wa siku. Ni afisi ya mtandao na matumaini tasa.
Wizara ya usalama wa ndani ndio jumba la makatuni wakubwa zaidi. Hapa ni siasa za kutisha watu kila kukicha.
Nimeskia kwenye mitandao kuwa ndugu Joseph Nkaissery huenda akawanyang’anya viongozi wote wanaozungumzia kifo cha Juma walinzi. La haula walakwata! Wakenya wote kwa ujumla hawana walinzi kwa maana asilimia kubwa ni maskini. Walinzi wetu ni Mwenyezi Mungu. Je, Nkaissery, uko tayari kushindana na ulinzi wa Mungu ukitumia ulinzi wako wa vitisho? Wakenya wanataka kujua ni nani aliyemuua Jacob Juma. Usijaribu kutisha wakenya ilhali wao ndio walipa ushuru. Wao ndio wanaokulipa mshahara wako. Wao ndio wanaokupa hiyo nafasi ya kujivinjari. Iweje badala ya kuwatumikia unawatishia kila mara unapofungua kinywa chako?
Sisi wakenya ndio tuliowaandika kazi, na ni sisi wakenya ndio tutakaowafuta kazi mwaka wa kuwanyoa na wembe bila maji, mwaka wa 2017!
Tangu Kenya kujinyakulia uhuru wake, hamna kesi hata moja iliyochaghuzwa kikamilifu hadi tamati yake na polisi wetu.
Wakenya shujaa kama Robert Ouko, Tom Mboya, Pio Gama Pinto, Oscar Kingara, John Oulu, Mellitus Mugabe Were, Mukabana miongoni mwa wakenya wengine wengi waliouawa kinyama na kuzikwa katika makaburi ya siri.
Wengi waliuawa na miili zao kutupwa ili kufuta ushahidi wa mauaji.
Wamewauawa Mashekhe na vijana Pwani ya Kenya, wameuawa vijana na wazee kaskazini mwa Kenya, Nairobi na maeneo mengine mengi nchini. Mauaji yamekuwa kama chakula cha kila siku tangu serikali hii ya kizazi kipya kuingia uongozini.
Wakenya wengi wameuawa na kuonekana kama jambo la kawaida. Nani aliyemuua Meshack Yebei? Njuguna Njuguna, Sheikh Aboud Rogo, Maina Ndiambo, Mbunge wa Kabete George Muchai, Abubakar Makaburi, Father John Kaisser, Sheikh Ibrahim, Mutula Kilonzo, George Saitoti, Orwa Ojode, Otieno Kajwang, Stephen Mukabana, Sheikh Samir Khan, Virginia Nyakio miongoni mwa wakenya wengine wengi walioangamizwa? Wako wapi hawa wanaojiita wachunguzi wa polisi? Wakenya tutauawa moja baada ya mwingine hadi pale tutakapo fumbua macho na kujua kuwa adui wa taifa hili ni uongozi mbaya. Hiyo siku ni 2017.
Standard Digital

Leave a Reply

Your email address will not be published.Don't Miss