mohaBy Mohamed Ali

Kizazi chenye kinyongo ndicho kinachozaliwa hapa nchini.

Kizazi kinacho abudu na kuongozwa na ukabila. Yanayojiri katika chuo kikuu cha Moi huko Eldoret ni ishara ya akili ndogo kutaka kutawala akili kubwa. Ishara ya viongozi kupasukiwa na akili na kusalia kufikiria kijinga. Ujinga wa tule sisi wahangaike wao. Inapofika wakati ambapo wasomi wanakuwa wakabila wakubwa nchini basi enyi wakenya wenzangu jihadharini maana twaelekea pabaya.

Chuki imetia mizizi akilini mwa mwanadamu. Sehemu kubwa ya chuki huenda hata ikawa imetiwa katika mfumo wote wa utendaji wa akili. Nashangaa kuwaona viongozi wakiandamana kupinga uteuzi wa mtu fulani sababu sio wa kabila lao. Wanaoongoza haya maandamano ni watu waliopata elimu kupitia vyuo vya humu nchini, lakini matendo yao na maamuzi yao hayana tofauti na utawala wa vijijini mahala ambapo chifu ndie mkweli kila mara hata akitamani bibi yako.

Kila asubuhi niamkapo nasikitika kuyaona mambo yakichafuka hapa nchini. Baadhi ya viongozi hawajali umoja wa taifa hili ila haja yao kuu ni kuchukua nguvu za utawala kuleta vurugu. Nchini Kenya matajiri ni wezi wenye nguvu, wamejifanya kana kwamba wao ni Mungu wa maskini.

Kenya tayari imetoka katikamfoleni ya amani, na inakoelekea ni kutumbukia kwenye bahari yenye mamba. Leo twajifanya waumini si kwa kupenda ila kwa kujilazimisha. Maombi pia yafanywa kikabila na kisiasa Kenya. Wahubiri wanajifanya wasafi. Tena nasema wahubiri wa dini zote wamekuwa kama mapaka, kazi yao kung’ang’ania senti za viongozi utadhani pakiti ya maziwa.

Leo wahubiri wanawaombea viongozi kuwa marais. Mie kila siku najiuliza mbona wasijiombee wao kuwa marais au wabunge? Leo wahubiri wanawaombea wezi wa taifa wanaojificha chini ya mwamvuli wa waheshima. Leo tunawaombea wauaji wazidi kutuua. Leo tunawaombea wabakaji wazidi kubaka dada na mama zetu. Leo tunawaombea wafisadi wazidi kufilisha taifa na kukamua tone ya mwisho ya damu iliyosalia miilini mwa wakenya.

Jamani nauliza hawa wahubiri, wanahubiri neon au meno. Mungu amewaalaani wote wanaotumia dini kama daraja la ukabila. Kabila letu ni la Maskini. Ni kabila la Majengo, Mathare, Kibera, Korogocho, Garissa, Mandera, Wajir, Tana River, Mpeketoni, Mombasa, Kapenguria hadi hapo ulipo au alipo nduguyo maskini.

Kutokana na ukabila na malipo duni sisi ndio wenye kuzifanya kazi zote ngumu kuwafurahisha wezi hawa wakabila. Ni sisi wenye kuwafuga kuku, ng’ombe na mbuzi zao zenye nyama tamu. Sisi ndio wenye kubeba mawe na kokoto kwenye majengo makubwa na manyumba manene yao. Ni sisi tulioijenga Ikulu inayoshidaniwa kila kukicha.Tulijenga Jela ya Kamiti, Lang’ata, Kondele na zinginezo kujifunga wenyewe badala ya kuwafunga wao. Ni sisi wenye kuzijenga barabara zinazopitiwa na magari mazuri ya matajiri hao wahuni wanaojiita viongozi.

Ni sisi madereva wao. Ni sisi wenye kuzinjenga kuta ndefu zizungukazo makaazi ya matajiri. Mbwa wao wanene na wakali twawapa chakula. Twawaandalia chakula matajiri hotelini na nyumbani mwao huku tukiwalea watoto wao wachanga huku wetu wakihangaika barabarani wakiuza njugu na viazi vya karai. Ni watoto wetu wenye kuajiriwa kazi kama za polisi na jeshi wanaotuua na kuuawa huko Somalia wakitumikia maslahi ya viongozi wachache.

Kodi twailipia ili waishi maisha mazuri wakati wanatutumikia. Yaani kwa ufupi sisi wajenga nchi twadharauliwa sana na hawa majahiliya wa kizazi kipya. Ajabu ni sisi wenye kupiga kura kuwapa uwezo wanasiasa kutupora na kutudharau.

Nambari yetu walalahoi ni zaidi ya milioni arobaine! Hii yote ni kwa sababu ya ukabila. Ukabila “Tribalism” maana yake rahisi ni sisi na wao, sisi ni bora na wao hawana sehemu na sisi. Ukabila unasababishwa na ubinafsi wa watu katika kutekeleza majukumu ya maendeleo katika jamii ambayo ina watu wenye mtazamo, itikadi, dini, lugha na tamaduni tofauti.

Ukabila hujitokeza ndani ya nchi ambayo huwa na vikundi na makabila ambayo yanazungumza lugha tofauti na kusambaa katika maeneo mbalimbali. Tanzania kwa mfano ni nchi yenye makabila zaidi ya mia moja na ishirini ambayo huzungumza lugha tofauti lakini inaunganishwa na lugha kuu ya kiswahili ambayo hutumika katika mawasiliano hasa katika shughuli za maendeleo.

Kenya taifa la makabila arobaine na miwili imegawanya makundi makundi na kuachwa kuabudu ukabila hata zaidi ya Mungu. Serikali ya Kenya haina dini ila ukabila. Jeuri za wanasiasa wa Kenya kutosikiliza vilio vya wananchi wao na kupuuza jitihada mbalimbali zimeleta madhara makuu nchini.

Wakenya lazima tupinge fikra finyu za watu wachache ambao wanakuza udini na ukabila kwa sababu bado dini zetu zinatuanganisha katika mambo mengi ya maendeleo na hivyo hakuna haja ya kutengana kwa tofauti zetu. Enyi wakenya wakabila mlirogwa na nani tumtafute? Utengano ni udhaifu bali umoja ni nguvu, wakenya tutatue tofauti zetu na kuungana kwa pamoja kuleta maendeleo katika taifa letu. Mimi kabila langu ni Kenya. Je, wewe?